SIO HALISI: Tangazo Hili La Kazi USAID Ni Bandia

Mnamo Septemba 22, 2021, barua hii inayotangaza nafasi za ajira katika Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) ilichapishwa kupitia mtandao wa Facebook.

Barua hiyo iliyotumia nembo ya USAID ilitangaza nafasi za ajira mbali mbali jijini Juba, nchini Sudan Kusini. Ilitoa mwaliko kwa Wakenya na wananchi wa nchi zinazoendelea kutuma wasifukazi na barua za kuomba kazi. Maombi ya kazi yalikuwa yatumiwe naibu afisa mtendaji mkuu wa USAID-Ampath Sudan Kusini kupitia barua pepe kabla ya Septemba 24, 2021 saa kumi na moja alasiri, saa za Afrika Mashariki.

Maelezo ya picha hayapo.

Siku mbili kabla ya barua hiyo kuchapishwa na mtumiaji wa Facebook kwa jina Yegama Waka Yegama, USAID lilikuwa limewatahadharisha watu kuhusu tangazo hilo la kazi. Hii iliashiria kuwa hiyo haikuwa mara ya kwanza kwa barua hiyo kuchapishwa mtandaoni. Kupitia akaunti yake rasmi ya Twitter, shirika la USAID Sudan Kusini lilisema kuwa barua hiyo ilikuwa bandia.

Piga Firimbi haikuweza kuthibitisha ni nani aliyeandika barua hiyo au kutangulia kuichapisha mtandaoni. Hii si mara ya kwanza kwa matangazo bandia ya nafasi za ajira katika shirika la USAID kuchapishwa. Mnamo Machi, 2020, tangazo bandia la nafasi za ajira zaidi ya 3,000 nchini Kenya lilichapishwa kwenye mtandao wa Facebook. Kama hapo kabla, USAID liliwatahadharisha watu na kuonya kuwa hiyo ilikuwa ni njama ya utapeli.

Usihadaiwe au kutapeliwa. Nafasi zote za ajira za USAID huchapishwa kwenye tovuti rasmi ya USAID, mitandao rasmi ya kijamii ya USAID au tovuti ya Ubalozi wa Marekani katika nchi husika. Kwa mfano kuhusiana na tangazo bandia tuliloliangazia la nafasi za ajira nchini Sudan Kusini, tangazo hilo lingechapishwa hapa kama lingekuwa la kweli.

Tafadhali kuwa makini unapokumbana na matangazo ya nafasi za ajira mitandaoni. Jihadhari hasa na matangazo yanayokuhitaji kulipia ada ya kutuma maombi ya kazi. Kabla ya kuchukua hatua yoyote, hakikisha umetembelea tovuti au mitandao rasmi ya kampuni au shirika linalodaiwa kuwa na nafasi za kazi, na kuthibitisha kuwa nafasi hizo ni za kweli. 

Makala hii ni sehemu ya makala za Africa Uncensored za kuhakiki ukweli wa taarifa zinazosambaa mitandaoni kupitia WhatsApp, Facebook, Twitter. Imehaririwa na Kabugi Mbae.

Add comment

Your email address will not be published.

Linda Ngari

Linda is a fact-checking and data journalist. She is currently the Piga Firimbi editor. She is passionate about acquiring and utilising OSINT tools and skills to tell stories that matter to a modern day tech-savvy audience in innovative ways.