UONGO: Picha Hizi Hazionyeshi Mauaji Ya Polisi Afghanistan

Ujumbe huu kwenye mtandao wa Twitter ulichapishwa Septemba 5, 2021. Unaonyesha picha za mauaji ya Banu Negar, anayedaiwa kuwa afisa wa polisi katika mkoa wa Ghor, Afghanistan. Inadaiwa Negar alikuwa mjamzito na mauaji yake yalitekelezwa mbele ya familia yake.

Kwenye ujumbe huu wa pili, picha inayosemekana kuwa ya Negar ilichapishwa ikiwa na madai sawia na ya awali.

Je, kati ya picha hizi mbili, ni gani iliyo halisi? Na je, madai yenyewe ni ya kweli?

Katika makala hii ya kuhakiki ukweli wa taarifa, Piga Firimbi inachanganua picha hizi ili kudhibitisha ukweli.

Hadi kufikia wakati huo, Taliban liliripotiwa kuzidi nguvu na kuchukua mamlaka ya Mkoa wa Panjshir. Huu ndio ulikuwa mkoa wa mwisho na wa 34 nchini Afghanistan kutwaliwa na Taliban.

Uchunguzi wa picha ya kwanza unaonyesha kuwa ilichapishwa Januari 19, 2020 kulingana na ujumbe huu wa Twitter. Inadai kuwa, mwaka huo, kundi la Taliban liliwaua watu sita kutoka kwa familia moja katika mji wa Andkhoy, Afghanistan.

Uchunguzi wa picha hii ya pili unaonyesha kuwa imechapishwa mara kadha kati ya Septemba 5, 2021 na sasa, baada ya mauaji ya Negar.

BBC, kwa mfano, ilichapisha makala kuhusu mauaji haya. Ilisema kuwa Banu Negar aliuawa mbele ya familia yake kwenye nyumba yao Firozkoh, makao makuu ya mkoa wa Ghor, Afghanistan. Kundi la Taliban lilikanusha kuhusika na mauaji hayo.

Familia ya Negar ilisema kuwa marehemu alikuwa na ujauzito wa miezi minane wakati alipouawa. Taarifa zaidi kuhusu mauaji ya polisi huyu hazikubainika kwani mashahidi wa tukio hilo walikataa kuongea kwa kuhofia usalama wao.

Kwa mujibu wa uchanganuzi wetu, picha ya kwanza inayodai kuonyesha mauaji ya Negar ni ya UONGO na inapotosha. Picha ya pili ndiyo ya kweli na inaonyesha sura halisi ya polisi aliyeuawa.

Makala hii ni sehemu ya makala za Africa Uncensored za kuhakiki ukweli wa taarifa zinazosambaa mitandaoni kupitia WhatsApp, Facebook, Twitter au Telegram. Imehaririwa na Kabugi Mbae.

Add comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *