SIO HALISI: Tangazo Linalodai Kuwafadhili Vijana Kifedha Ni Ghushi

Ujumbe huu unaodai kutoa ufadhili wa fedha kwa vijana kupitia mradi wa ‘National Youth Empowerment Fund’ umekuwa ukisambaa kwenye mtandao wa WhatsApp.

Mradi huo unadai kuwapa wanafunzi na wanabiashara pekee wenye umri wa miaka 13-65 kati ya shilingi 150,000-700,000. Tovuti hii imejumuishwa kwenye ujumbe huo ili kuwawezesha wanaotimiza masharti kusajili.

Hata hivyo, tovuti hio inaashiria utata kwani unapoifungua, jina la mradi linabadilika kutoka ‘National Youth Empowerment Fund’  hadi ‘Presidential Youth Empowerment Scheme’. Jina hili ni sawa na lile la mradi uliozinduliwa na rais wa Nigeria Muhammadu Buhari mnamo Oktoba 12, 2020, almaarufu P-YES.

Vilevile, tovuti hio inawataka watu kuandikisha taarifa zao za kibinafsi zikiwemo nambari za simu na anwani za barua pepe. Hii inaashiria uwezekano wa njama ya utapeli mtandaoni kupitia mtindo wa ‘Phishing Scam’, ambapo taarifa za kibinafsi hukusanywa na kutumika kwa ulaghai.

Zaidi ya hayo, usajili unawaagiza watu kuwajulisha familia na marafiki kuhusu mradi huo kwa kuwatumia anwani ya tovuti hiyo kupitia vikundi vya WhatsApp.

Agizo hilo pia linaashiria utapeli wa mtandaoni unaojulikana kama ‘Engagement Bait Scam’. Aina hiyo ya utapeli huo huhusisha sharti la kusambaza anwani ya tovuti kupitia mitandao ya kijamii kama vile WhatsApp, Facebook, Twitter au Telegram. Lengo la matapeli huwa ni kuwafikia watu wengi inavyowezekana kupitia jamaa na marafiki za wanaojisajili.

Hapo kabla, Piga Firimbi ishawahi kuchapisha makala iliyodhibitisha kuwa taarifa zinazodai kuwafadhili kifedha vijana wa nchi mbalimbali kupitia mradi wa P-YES ni bandia. Kadhalika kulingana na makala ya 211 Check, mradi huo haujaidhinishwa na nchi nyingine yeyote isipokuwa Nigeria.

Kwa hiyo, uchapishaji wa bendera za nchi za Kenya, Uganda, Afrika Kusini pamoja na nembo zinazowakilisha mataifa ya Nigeria na Ghana katika tovuti hiyo unapotosha.

Ni muhimu kuzingatia kuwa tovuti halisi ya mradi uliozinduliwa na Rais Buhari ni p-yes.net na sio power.claimonline.co.ke

Uchunguzi zaidi unaonesha kuwa tovuti halisi ya mradi huo ilisajiliwa Aprili 2021, ilhali tovuti bandia ilisajiliwa Novemba 2021.

Hitimisho la Piga Firimbi ni kuwa tovuti ya power.claimonline.co.ke iliyosajiliwa nchini Kenya ni ghushi na ahadi inayotoa ya ufadhili wa kifedha si ya kweli. 

Makala hii ni sehemu ya makala za Africa Uncensored za kuhakiki ukweli wa taarifa zinazosambaa mitandaoni kupitia WhatsApp, Facebook, na Twitter. Imehaririwa na Kabugi Mbae.

Add comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *