UONGO: Raila Odinga hakuchapisha ujumbe unaohimiza watu kumpigia kura mpinzani wake William Ruto

Ujumbe unaompigia debe Naibu Rais wa Kenya William Ruto na unaodaiwa kuandikwa na kiongozi wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM) Raila Odinga umekuwa ukisambaa mitandaoni, hasa Facebook. Katika ujumbe huo, Raila Odinga ambaye ni mpinzani wa kisiasa wa Ruto, anasema: “Nimechoka. Mpigieni kura Ruto.”

Haya yanajiri wakati wawili hawa wakiwa tayari wameonyesha nia ya kuwania urais katika uchaguzi mkuu mnamo Agosti mwaka 2022. Huku ikiwa imesalia chini ya mwaka mmoja kwa uchaguzi huo kufanyika, Odinga na Ruto wamekuwa wakiendesha kampeni zao katika maeneo mbali mbali nchini Kenya wakiandamana na wandani na wapambe wao wa kisiasa kutoka vyama vya ODM na United Democratic Alliance (UDA) chake William Ruto. Baadhi ya kauli za wanasiasa wanaowaunga mkono Odinga na Ruto zimekuwa zikichapishwa kwenye mtandao wa Twitter.

 

Piga Firimbi ilichanganua ujumbe unaosemekana kuchapishwa na Raila Odinga kupitia akaunti yake rasmi ya Twitter.

Ujumbe huo ambao unaonyesha kuwa ulichapishwa Agosti 8, 2021 haupo kwenye akaunti ya Odinga ya Twitter. Jumbe zilizochapishwa tarehe hiyo kupitia akaunti ya Raila Odinga ni mbili tu: Ujumbe mmoja ulimpongeza mwanariadha Eliud Kipchoge kwa kushinda medali ya dhahabu kwenye mbio za Olimpiki na wa pili ulizungumzia ziara ya Odinga mjini Mombasa.

Hakuna tangazo lolote ambalo Raila Odinga ametoa kuashiria kuwa ameghairi nia yake ya kuwania urais mwaka ujao. Hili pia halijatangazwa na vyombo vya habari nchini Kenya. 

Hitimisho la Piga Firimbi ni kuwa ujumbe anaodaiwa kuandika Raila Odinga akiwahimiza watu wampigie kura mpinzani wake William Ruto ni wa UONGO.

 

Makala hii ni sehemu ya makala za Africa Uncensored za kuhakiki ukweli wa taarifa zinazosambaa mitandaoni kupitia WhatsApp, Facebook, na Twitter. Imehaririwa na Kabugi Mbae.

Add comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *